Mahakama yaagiza NABII TITO afike mahakamani







MAHAKAMA ya wilaya ya Dodoma imeagiza kufikishwa mahakamani Mkazi wa mtaa wa Ng’ong’ona Manispaa ya Dodoma Tito Machibya, maarufu kama ‘Nabii Tito’ (45) anayeshtakiwa kwa kosa la kujaribu kujiua kwa kutumia wembe,ili kusikiliza shauri lake.

Hatua hiyo ilifikiwa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha baada ya kupata taarifa kuwa Nabii Tito hakufikishwa mahakamani kutokana na kuwa bado anaendelea kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa akili unaomkabili Taasisi ya afya ya akili Mirembe Isanga.

Kabla ya kutoa agizo hilo, Hakimu huyo aliwahoji askari magereza waliokuwepo ni kwanini mshtakiwa huyo hajafikishwa Mahakamani ambapo mmoja wao alijibu kuwa Nabii Tito bado yupo kwenye kitengo cha ‘Bloodmore’ Mirembe anaendelea na matibabu ya ugonjwa wa akili bado hajarudishwa mahabusu.

Askari magereza huyo ambaye hakutaja jina lake, alisema kuwa tangu mahakama ilipoamuru Nabii Tito afanyiwe vipimo vya kujua kama ana ugonjwa wa akili au laa, mwezi Februari mwaka huu bado mtuhumiwa huyo hajamaliza siku za uchunguzi wa vipimo hivyo, na kwamba hayupo mahabusu kwenye gereza la Isanga.

Kufuatia majibu hayo, Hakimu Karayemaha alisema mshtakiwa huyo anapaswa kufikishwa mahakamani ili kuendelea na kesi yake au apate maelezo kamili ya kwa nini hafikishwi mahakamani.

“Kama kuna ulazima wa kutokufika mahakamani basi niletewe maelezo rasmi yanayomkwamisha mshtakiwa huyu kufika mahakamani, Nimeamini kuwa mtuhumiwa yupo mirembe kwa kuwa aliyetoa maelezo hayo ni askari magereza,”alisema Karayemaha.

Aliagiza April 5, mwaka huu mtuhumiwa huyo afike mahakamani kuendelea na kesi yake au apate taarifa rasmi za kwa nini hafiki mahakamani.

“Nataka aripoti siku hiyo si inakuja kutajwa tu?,Naahirisha kesi hii hadi April 5 mwaka huu ambapo itatajwa tena,”alisema Hakimu huyo.

Jana ni mara ya pili Nabii Tito hakuweza kufika mahakamani kuendelea na kesi yake kutokana kufanyiwa vipimo vya ugonjwa wa akili Mirembe.

Nabii Tito anashtakiwa kwa kosa la kutaka kujiua kwa kujikata na wembe na kujijeruhi kwenye maeneo ya tumbo Januari 25, mwaka huu katika mtaa huo wa Ng’ong’ona alipokwenda kukamatwa na polisi.

Post a Comment

0 Comments