Mbowe atoa sharti kwa Zitto





Image result for mbowe


SIKU chache baada ya Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kusema ataishawishi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuibeba hoja yake ya kuwasilisha mpango mbadala wa bajeti bungeni, kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe ametoa sharti kwa mbunge huyo.

Jumatatu, Zitto aliiambia Nipashe kuwa amepanga kuishawishi kambi hiyo kuichukua hoja yake hiyo ya kuwasilisha mpango mbadala kuhusu sera za kibajeti ili iwekwe katika taarifa yake wakati wa mkutano ujao wa Bunge la Bajeti.

"Nitatumia kanuni ya majadiliano bungeni, nitaandika rasmi na kuchangia. Pia nitaishawishi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuichukua hoja hiyo na kuiweka katika taarifa yake bungeni," alisema.

Hata hivyo, Mbowe alipotafutwa na Nipashe jana mchana kuzungumzia suala hilo, alisema hajapokea rasmi maombi ya Zitto na akamtaka Mbunge huyo wa Kigoma Mjini kuandika barua kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja yake hiyo kama kweli anataka iunganishwe kwenye taarifa ya kambi hiyo wakati wa Bunge la Bajeti.

"Nimesikia suala hilo kupitia vyombo vya habari kwamba Mheshimiwa Zitto ana hoja hiyo lakini hatujapata barua rasmi kutoka kwake," Mbowe alisema na kueleza zaidi:

"Kambi inafanya kazi kwa ushirikiano na vyama vyote. Kama Mheshimiwa Zitto ana suala hilo, atuandikie rasmi tulione. Hatuwezi kumjibu kwa kusikia kupitia vyombo vya habari."

Jumapili, Zitto alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuweka bayana kuwa amejipanga kupeleka bungeni mpango mbadala kuhusu sera za kibajeti akidai mpango wa sasa wa bajeti ya serikali umejikita kwenye maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu.

Zitto (41), alisema hoja yake hiyo imelenga kuunda mpango mwingine mpya utakaosimamia masuala ya uchumi shirikishi unaozalisha ajira pamoja na kuhakikisha kilimo na viwanda vinavyoongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo vinapewa kipaumbele.

Vitu vingine ambavyo alisema vinapaswa kupewa kipaumbele ni usalama wa chakula na lishe pamoja na huduma bora za kijamii hususani maji, elimu na afya.

“Juzi serikali imeainisha vipaumbele vya kibajeti kwa mwaka 2018/19. Masuala ya watu hususani kilimo, maji hayamo kwenye vipaumbele hivyo," Zitto alisema na kufafanua zaidi:

"Ni rai yetu kwa serikali ijitazame katika eneo hilo, ikae chini na kuja na mpango mpya utakaojikita katika masuala ya watu na siyo kama mpango huu wa sasa unaojikita kwenye vitu tu.

“ACT-Wazalendo tutahakikisha tunaupinga bungeni mpango huu wa bajeti wa sasa ili uandaliwe upya kwa sababu huu uliopo unawaacha kando kwa asilimia 70 Watanzania, tunataka tuwe na 'balance' (uwiano) ya vipaumbele vya kujenga nchi na vya kujenga taifa ili tuhakikishe vitu vya muhimu kama elimu, kilimo, afya na vitu vingine vinavyowahusu watu moja kwa moja vinaguswa na kupewa kipaumbele."

Wiki iliyopita serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango iliwasilisha kwa wabunge mapendekezo yake kuhusu ukomo wa bajeti na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2018/19.

Dk. Mpango alisema bajeti ijayo ambayo itakuwa ya tatu kwa serikali ya awamu ya tano inatarajia kuwa Sh. trilioni 32.476. Kati yake, Sh. trilioni 20.468 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 63 ya bajeti na Sh. trilioni 12.007 zitatumika kwa shughuli za maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti.

Waziri huyo alisema miradi kielelezo itakayopewa msukumo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge kiasi cha Sh. trilioni 1.4, kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege ya pili aina ya Dreamliner-Boeing 787, ununuzi wa ndege moja mpya aina ya Bombadier Dash 8 Q400 na kuanza uendeshaji wa ndege mpya Boeing 787 na Bombardier CS 300, zikitengewa Sh. bilioni 495.6.

Pia alisema Sh. bilioni 700 ambazo ni fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kambi na ofisi za wafanyakazi, ujenzi wa bwawa na ujenzi wa njia kuu za kupitishia maji katika mradi wa Stieglers' Gorge.

Post a Comment

0 Comments