Bunge la Zambia limemsimamisha kazi Waziri wa Jimbo la Lusaka, Bowman Lusambo kwa muda wa mwezi mmoja baada ya kumchapa kibao mbunge Chishimba Kambwili wakiwa bungeni.
Spika wa Bunge hilo amesema ni jambo la kawaida wabunge kutumia lugha isiyofaa na kuleta mizozo lakini kwa kitendo cha Waziri kumpiga kibao mbunge ni kitendo kisicho vumilika.
Patrick Matibini ambaye ni spika wa Bunge hilo amesema kitendo hiko kilifanyika Oktoba mwaka jana, na kuongezea kwamba tabia hiyo haikubaliki kamwe.
“Hili ni Bunge la heshima, nina wajibu wa kuhakikisha kwamba heshima na haiba ya Bunge inalindwa na inahifadhiwa wakati wote,” amesema spika huyo.
Hivyo kufuatia adhabu hiyo, Waziri Lusambo atasitishiwa baadhi ya huduma zinazotolewa bungeni kama marupurupu na mshahara kwa muda wa kipindi chote atachokuwa anatumikia adhabu hiyo.
Aidha imeelezwa kuwa mbunge huyo aliyepigwa kibao amekuwa akiwatukana maofisa wa Serikali kwa tuhuma za rushwa tangu atolewe kuwa Waziri wa Mawasiliano mwaka 2016, japo Serikali imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.
Hata hivyo imeelezwa kuwa Waziri huyo alichukua sheria hiyo mkononi ya kumchapa kibao mara mbili baada ya kuona mbunge huyo anazungumza uongo juu ya Serikali.
0 Comments