NAMNA TAIFA STARS ILIVYOIPELEKA MBIO BENIN, WADHAMINI SERENGETI WAWEKA NENO LAO

 
 
 
 
 
 
 
 
 
Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ambao ni wadhamini wakuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, wameelezea kuvutiwa na kiwango cha soka kilichoonyeshwa na timu hiyo katika mchezo wake dhidi ya Benin.

Jumapili iliyopita, Taifa Stars ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya taifa ya Benin uliochezwa katika jijini la Porto-Novo nchini Benin. 

Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, Ceaser Mloka, amesema kiwango cha Taifa Stars kimekuwa kikiridhisha na kutia moyo tangu kampuni hiyo iingie udhamini nayo.

Alisema ni jambo la kutia moyo kwamba tangu SBL itoe udhamini, Taifa Stars haijapoteza mechi yoyote, iwe ni nyumbani au ugenini.

“Tukirejea kwenye mechi ya Jumapili dhidi ya Benin, kama Benin wasingepata penalti ni wazi kuwa Taifa Stars wangeibuka washindi,” alisema.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa, Taifa Stars walicheza vizuri katika mechi hiyo pamoja na kwamba Benin wako mbele yao katika nafasi za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Kwa mujibu wa viwango vya Fifa, Benin inashikilia nafasi ya 86 huku Tanzania ikishikilia nafasi ya 136.

Ceaser alisema kukosekana kwa wachezaji muhimu wawili wa Taifa Stars Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kutokana na kuwa majeruhi pia kumeathiri matokeo huku akisisitiza kuwa timu inaendelea kuimarika.

Mei, mwaka huu, SBL iliingia mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) wa thamani ya shilingi bilioni 2.1 ambao uliifanya kuwa mdhamini  mkuu wa Taifa Stars.

Udhamini huo ni wa mara ya pili kwa SBL kuiunga mkono timu ya taifa baada ya kampuni hiyo kufanya hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu ilipoidhamini timu hiyo kati ya mwaka 2008 hadi 2011.

Post a Comment

0 Comments