KLABU
ya Simba imemualika Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.
Harrison Mwakyembe katika mkutano mkuu wa wanachama utakaofanyika kesho
kuanzia Saa 4:00 asubuhi kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Dar es
Salaam.
Mkuu
wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Hajji Manara ameseam
kwamba wanataka kuutumia mkutano huo kumtangaza mshindi wa zabuni ya
uwekezaji katika klabu yao.
Miezi
miwili iliyopita klabu hiyo ilitangaza zabuni kwa wanachama wenye uwezo
na mtaji kuanzia Sh. Bilioni 20 kujitokeza na kufanya uwekezaji katika
klabu hiyo katika mchakato wa mabadiliko ya muundo wa uendeshaji hadi
kuwa wa hisa.
Alisema anaamini huo utakuwa ni mkutano wa kihistoria kwasababu wanakwenda kubadilisha muundo.
“Tunapokwenda
kubadilisha mfumo wa uendeshaji tunategemea klabu yetu itakuwa ni
tajiri na kuwekeza kwenye miundombinu, itakuwa ina uwezo wa kununua
wachezaji bora watakaowezesha kuwa na ligi bora Tanzania na kushinda
mataji mengi klabu bingwa Afrika,”alisema.
Awali,
klabu hiyo ilisema mwekezaji atamiliki asilimia 50 ya hisa huku
asilimia 10 zikitarajia kugawiwa kwa wanachama hai na nyingine 40 kuuzwa
kwa wanachama.
Tayari
mfanyabiashara na mfadhili wa Simba Mohamed Dewji aliwahi kuonyesha nia
ya kuwekeza iwapo tu atapewa asilimia 50 ya hisa, ingawa hata hivyo,
kesho itajulikana kama atakuwa yeye au wengine kutokana na vigezo
vilivyokuwa vimewekwa.
Hata
hivyo, kazi bado ipo kwa Simba kwani serikali kupitia Baraza la Michezo
la Taifa (BMT) limefanya marekebisho ya kanuni zake na juzi kutoa
waraka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unaotoa maelekezo ya
ununuaji na uuzwaji wa hisa za klabu au Chama cha Michezo.
Marekebisho
yaliyopo ni kwamba Vyama au klabu zilizoanzishwa na wanachama vikiamua
kuuza hisa zake vinapaswa kutenga asilimia 51 kwa ajili ya wanachama na
asilimia 49 kwa wanaotaka kununua.
Pia,
wanatakiwa kupitia kwenye mamlaka ya mitaji na masoko ili kuidhinishwa
na baadaye kurudi kwenye soko la hisa ili kufuata taratibu za uuzwaji
na ununuaji.
Manara
alisema tayari wamepata taarifa hiyo kutoka TFF na wanaendelea na
mazungumzo na Dk. Mwakyembe kuhusu taratibu hizo mpya na namna ya
kubadili kanuni wakati wakiendelea na mchakato wao wa kutangaza
mwekezaji.
0 Comments