MSHAMBULIAJI
chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Yohana Oscar Nkomola amejiunga na
mabingwa wa Bara, Yanga SC kwa mkataba wa miaka miwili.
Nkomola
anayesimamiwa na akademi ya Cambianso ya Dar es Salaam amesaini mkataba
huo mapema wiki hii kabla ya kwenda Kenya na kikosi cha Tanzania Bara
kwenye michuano ya Kombe la CECAFA Challenge.
Kwa
kusaini Yanga, Nkomola anakuwa mchezaji wa tatu kutoka kikosi cha timu
ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys
kilichoshiriki Fainali za Vijana za U-17 Afrika nchini Gabon mwezi Mei
mwaka huu.
Wengine
ni kipa Ramadhani Kabwili na kiungo Mussa Said ambao wote wanasajiliwa
kama wachezaji wa kikosi cha pili kinachoundwa na vijana chini ya umri
wa miaka 20, watakaokuwa wanakomazwa pia kikosi cha kwanza.
Septemba
mwaka huu Nkomola alisema amefaulu majaribio katika klabu ya Etoile du
Sahel ya Tunisia na atatakiwa kuanzia timu ya vijana hadi atakapofikisha
umri wa miaka 18 Aprili mwakani ndipo atasaini mkataba rasmi na kuanza
kuchezea timu ya wakubwa.
Hata hivyo, wamiliki wa mchezaji huyo, Cambianso wameona bora ajiunge na Yanga kuliko kurejea Etoile du Sahel.
Tayari
Nkomola ameanza kukomazwa kwenye timu ya wakubwa ya Tanzania na
alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars ikitoa sare za 1-1 katika mechi
zake mbili zilizopita dhidi ya Malawi Dar es Salaam na Benin mjini
Coutonou.
Na
wakiwa kambini kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Malawi, Nahodha wa
Taifa Stars, Mbwana Samatta alimsifu kijana huyo na akamtabiria atafika
mbali akiongeza juhudi.
0 Comments