TAASISI ya Sekta Binafsi (TPSF), imeridhishwa na maamuzi ya Rais John Magufuli ya kuwapa watendaji wa serikali siku saba kutoa majibu ya malalamiko yaliyotolewa na wafanyabishara katika Mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Jumatatu.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa sekta binafsi imevutiwa na namna Rais Magufuli alivyoongoza kikao hicho na kuonyesha kuguswa na changamoto zinazoikabili sekta binafsi nchini.
"Ukiangalia matatizo mengi kutoka sekta binafsi yaliyoongewa si ya kisera, ni matatizo yanayohitaji maamuzi na uwezeshaji," alisema Simbeye.
"Ndio maana Rais alisema kwa uchungu kuwa serikali ina wajibu kuwasaidia watu kumaliza matatizo ya huduma kama umeme maji na barabara."
Simbeye alisema urasimu umekithiri miongoni mwa watendaji wa serikali ambapo mambo mengi yanachelewa bila sababu za msingi, Aidha, alisema kuna haja ya kubadilishwa sera ya kodi ili iache kumkandamiza mfanyabiashara.
"Tulizungumzia urasimu uliokithiri serikalini, mtu anachelewesha tu... hataki kuamua, hataki kufanya chochote bila maelezo ya kueleweka," alisema zaidi Simbeye.
"Rais amesikiliza watu wote na ametoa wiki koja kila kitu kifanyiwe kazi au watu wa serikali kuja na majibu... sijawahi kuona uamuzi mzuri kama huu."
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu, Prof. Faustine Kamuzora alisema ofisi ya Waziri Mkuu ipo tayari kuhakikisha mazingira ya biashara nchini yanakua mazuri na watasimamia sera na kanuni.
"Maelekezo ya Rais yapo wazi, kanuni na sheria zote zimeshabainishwa katika kitabu," alisema Prof. Kamuzora. "Tunajitahidi shughuli zote za kiuchumi ziwe zinaongeza tija na wafanyabishara wanatengenezewa mazingira ya kupata faida."
Prof. Kamuzora alisema kwa sasa Watanzania wanaongezeka kwa kasi na uchumi kadiri unavyokua soko linakua kubwa.
Aidha, katibu mkuu huyo alisema kuna ongezeko la teknolojia na vijana wenye ujuzi ambao wakipewa fursa wanakua wajasiriamali wazuri.
0 Comments