KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mrundi Ramadhani Nsanzurwimo amesema kwamba anastahili lawama kwa kipigo cha 5-0 kutoka kwa Yanga jana. Mbeya
City jana ilichapwa 5-0 na mabingwa watetezi, Yanga SC katika mchezo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam,
Mzambia Obrey Chirwa akifunga mabao matatu na mzawa, Emmanuel Martin
akifunga mawili. Akizungumza
na Waandishi wa Habari jana baada ya mchezo huo, kocha Ramadhani
alisema kwamba amesikitishwa mno na matokeo hayo, kwani ni kinyume
kabisa matarajio yake. “Tulikuja
na mipango ya kushinda hii mechi, lakini tumeshindwa kufanikisha
mipango yetu na matokeo yake tumefungwa sisi, imeniumiza sana. Ila ndiyo
mchezo,”alisema. Kocha
huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Malawi amesema kwamba yeye ndiye
anastahili kubeba lawama za kupoteza mchezo huo, lakini anakwenda
kufanyia kazi mapungufu. Kipigo
hicho cha jana ambacho ni cha tatu mfululizo ikitoka kufungwa 1-0 mara
mbili, na Azam FC mjini Dar es Salaam na Simba mjini Mbeya, kinaifanya
Mbeya City ibaki na pointi zake 11 baada ya mechi 10 katika nafasi ya
tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu, sawa na Maji Maji walio nafasi ya nane. Mbeya City itateremka tena uwanjani Ijumaa wiki hii kumenyana na wenyeji, Singida United Uwanja wa Namfua.
0 Comments